"Watoto milioni 80 wapo hatarini"

Covid-19 yapelekea kusitishwa kwa utoaji wa chanjo kwa magonjwa mengine duniani

1422269
"Watoto milioni 80 wapo hatarini"

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema kuwa watoto milioni 80 chini ya umri wa mwaka 1 kati ya mataifa 68 wamehatarishwa kutokana na janga la COVID-19.

Mkuu wa shirika la watoto la UN amezungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kuhusu COVID-19 wa kila wiki kufuatia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)  Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Ameonya pia kuwa moja ya huduma muhimu za kiafya zilizovurugika kutokana na virusi ni chanjo ya watoto wachanga.

"WHO na UNICEF wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu tangu kuanza kwa mlipuko huu kuhakikisha vifaa muhimu vinawafikia wafanyikazi wa afya, wagonjwa na watoto ulimwenguni kote," alisema Tedros.

Fore aliongeza: "Watoto milioni 80 chini ya umri wa mwaka 1 wako katika hatari kwa sababu huduma za chanjo za watoto wachanga zimevurugwa sana katika nchi 68."

Akiongea kutoka New York kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliyofanyika huko Geneva, alisema: "Kampeni za chanjo ambazo huhamasisha chanjo ndani ya kipindikifupi zimevurugika pia,hasa chanjo za magonjwa ya ukambi na polio."

Mkuu wa UNICEF amesisitiza kuna sababu nyingi halali kwa nini juhudi za chanjo zimeathiriwa kwani nchi zimelazimika kusitisha kampeni kutokana na hitaji la kudumisha umbali wa mita moja kuepuka maambukizi ya corona.

Kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari, Seth Berkley, Mkurugenzi Mtendaji wa GAVI muungano wa chanjo alisema: "Hii ni data ya kutisha sana ambayo tunatangaza leo."

Mapema katika siku hiyo, Tedros alisema katika mkutano wa baraza kuu la WHO: "Tangu mwanzo wa janga hilo, WHO imefanya kazi mchana na usiku kuratibu majibu ya ulimwengu katika ngazi zote tatu za shirika, kutoa ushauri wa kiufundi, kuchochea mshikamano wa kisiasa, uhamasishaji rasilimali, kuratibu vifaa, na mengi zaidi.

"Tumeandaa zana za mawasiliano ya hatari kwa wazazi na watoto, wafanyikazi wa afya, waajiri, mashirika ya imani, na zaidi."

 Habari Zinazohusiana