Mkorogano baina ya Marekani na Iran

Mvutano na mkorogano baina ya Marekani na Iran imezidi kuchukua kina, matukio ya hivi karibuni yakipelekea mashariki ya kati kutingishika huku wadau wote wa kanda wakipiga mahesabu juu ya hatua watazochukua

Mkorogano baina ya Marekani na Iran

 Mvutano baina ya Iran na Marekani uliongezeka zaidi kufuatia Marekani kumuua kamanda wa jeshi la ulinzi wa mapinduzi ya İran, jenerali Kasim Suleiman na kisha Iran kulipiza kisasi kwa kulenga kwa makombora kambi za jeshi za Marekani nchini Irak. Suleiman katika siku za hivi karibuni alikuwa  uti wa mgongo wa Iran katika siasa za kikanda.  Jina la Suleiman lilipata umaarufu zaidi kama mratibu wa siasa za nje za Iran mara baada ya kuanza uasi katika mataifa ya kiarabu. Suleiman alitekeleza majukumu muhimu katika ajenda ya nchi yake huko Lebanon, Syria, Irak na Yemen alikuwa ndio mratibu mkuu wa makundi ya kisilaha ya kishia.Mbali na hayo Suleiman alifanikiwa kujijengea heshima ya kiutawala miongoni mwa makundi ya kijeshi ya kishia kutokea Lebanon hadi Yemen na katika siasa za ndani za Iran alijipatia umaarufu mkubwa kwa kiongozi wa kiroho wa nchi hiyo, Khameney pamoja na Rais Ruhani. Ikifikirwa majukumu aliyokuwa nayo Suleiman na mchango wake, inawezekana Iran ikaanza kupitia kipindi cha mtikisiko mzito.

SETA /  Mkurugenzi wa utafiti wa masuala ya Usalama Mwandishi Mwl. Dkt. Murat Yeşiltaş anachanganua kuhusiana na mada hii...

 

             Kuuliwa kwa Suleymani na muda mchache baadae Iran kulipiza kisasi vikali kunaweza kutafsiriwa kama siasa za mashariki ya kati kwa mwaka 2020 zitakuwa moto sana. Haifahamiki kama mvutano baina ya Marekani na Iran utakuwa ndio chanzo cha vita kamili miongoni mwa mataifa hayo mawili, lakini vita baridi iliyodumu kwa muda mrefu miongoni mwa mataifa hayo itazidi. Utawala wa Tehran mara baada ya kifo cha Suleiman ulijiapiza kulipa kisasi na muda mfupi baadae imetekeleza kiapo chake. Jamii ya Iran ambayo inapitia madhila kwa muda mrefu nayo iliungana na utawala na kujitokeza kwa wingi katika mitaa ya Tehran wakitoa kauli mbalimbali za viapo vya kisasi. Katika mitaa ya Baghdad nako zilisikika kauli za viapo vya kisasi kwa waliouawa pamoja na Kasim yaani Muhendis na wenzie.

Tumeshuhudia picha za video vya makundi mapya ya kijeshi yaliyoanzishwa makubwa na madogo nayo pia yakijiapiza kulipa kisasi. Bunge la Irak nalo kwa kauli moja limeamua pamoja na kutoa madaraka kwa serikali kuvifukuza vikosi vya jeshi la Marekani nchini Irak.

Irak ambayo ipo kwenye machafuko na mkorogano wa  muda mrefu haifahamiki ni jinsi gani itajikwamua katika mchafukoge hii. Raia wa Irak wanatambua kwamba mvutano na ushindani wa Marekani na Iran unaiingiza nchi yao shimoni kwa kuigeuza uwanja wa mapambano. Lakini hawana cha kufanya. Hawana kanuni yeyote itakayowawesha kuwa huru dhidi ya Marekani vilevile dhidi ya Iran.

Utawala wa Tehran uliitisha mkutano wa baraza la juu la usalama la nchi hiyo ambalo hukutana kwa nadra sana kwa masuala maalumu ya dharura, Mkutano huo ulihudhuriwa pia na kiongozi wa kiroho, Khameney. Serikali ya Iran ilipandisha  bendera ya rangi nyekundu katika minara ya misikiti, bendera hiyo ni katika alama muhimu  za imani ya kishia na inaashiria vita.

Utawala wa Tehran hali kadhalika umetangaza kujitoa katika kutekeleza makubaliano ya mkataba wa kimataifa wa nyuklia na kwamba itaendelea na urutubishaji wa madini ya Uranium. Pia waliongeza kwamba wataijibu vikali sana Marekani. Hatimaye katika kujibu mapigo Iran ikavurumusha makombora lukuki katika kambi za kijeshi zinazohifadhi askari wa Marekani na washirika wake nchini Irak. Ni vigumu sana kufahamu kwa sasa kama majibu hayo ya Iran yametosha kulipiza kisasi cha kuuawa kwa Suleiman. Suala la muhimu zaidi hapa ni jinsi gani Marekani nayo itajibu mapigo kwa Iran.

Hakika kuuawa kwa Suleimani kumepelekea kutingishika kwa mashariki ya kati. Wadau wote hivi sasa wanapiga mahesabu kutokana na makadirio yao ya kitachojiri baada ya kuuawa kwa Suleimani. Kwa hivi sasa unaweza kusema nchi pekee inayojaribu kutuliza jazba zilizopo ni Uturuki.

 Habari Zinazohusiana