Ni mpango kabambe uliosukwa kwa kutumia akili kubwa

Uchambuzi kutoka kwa mkuu wa kitivo cha elimu ya siasa wa chuo kikuu cha Ankara Yıldırım Beyazıt Prof. Dr. Kudret BÜLBÜL

Ni mpango kabambe uliosukwa kwa kutumia akili kubwa

Kazi za kitafiti za watafiti wa magharibi zinazohusiana kwa upande mmoja na ubeberu na kwa upande mwingine siasa, utamaduni, dini, makabila, antropolojia na vitu vingine vya jamii za mashariki  huitwa Orientalizm. Maana hii pia hujumuisha mtazamo hasi dhidi ya jamii za mashariki zinavyotazamwa kutoka nje, ambapo huonekana jamii zisizokuwa na hisia.

Kuhusiana na mada hii mkuu wa kitivo cha elimu ya siasa wa chuo kikuu chaAnkara Yıldırım Beyazıt Prof. Dr. Kudret BÜLBÜL anatufafanulia...

Katika dunia ya sasa  kazi za kiorentali hazijapotea. Isipokuwa zimebadilika kwa kiasi kikubwa.Jinsi zilivyokuwa zikifanyika mwanzo kwa watafiti wa magharibi kufunga safari kuelekea  mashariki na kufanya utafiti kihalisia, imeonekana hakuna umuhimu wa kufanya hivyo tena. Na hii ni kwa sababu  kadiri siku zinavyokwenda watafiti wa mashariki wamekuwa wakifanya tafiti hizi wao wenyewe. 

Hekaya yetu ya hazina ya miaka 200

Karibu kwa miaka 200 watafiti, wanafunzi, wataalamu na wanafunzi kutoka magharibi wamekuwa wakitumwa katika nchi kama Uturuki na Japan ambazo zimekuwa hazifungamani kikamilifu  na tamaduni za magharibi. Kwa sasa pia tumekuwa tukiona njia hii hii ikitumiwa.

Nchi za Afrika, Balkani, mashariki ya kati, mashariki ya mbali, Amerika ya kusini, nchi kama China na India  zimekuwa zikituma wataalamu wao kutoka vyuo vikuu kwenda nchi za magharibi.

Si wataalamu wa vyuo vikuu pekee bali hata maafisa kutoka wizara, mashirika, taasisi za kielimu, kiutamaduni, kihabari na kada nyingine mbalimbali wamekuwa wakitumwa nchi za magharibi kwa madhumuni ya kwenda kupata udhoefu.

Nchi hizi masikini zimekuwa zikitumia gharama kubwa kwa madhumuni hayo ya kutafuta udhoefu kutoka magharibi, ambako kunaonekana kuna sayansi na teknoloji ya hali ya juu.Kwa kufanya hivyo mataifa haya masikini yamekuwa yakiacha kutekeleza mambo mengi muhimu katika nchi zao, swali ni kwamba je madhumuni yao hayo ya kupata udhoefu yanafanikiwa ? Kwa kuwa ni miaka 200 sasa watu wamekuwa wakienda mataifa ya magharibi kwa ajili ya kupata elimu, hiyo inaweza kuonyesa madhumuni hayajafikiwa inavyohitajika.

Miaka ya vyuo vikuu “ Wajapan walichukua sayansi na teknolojia kutoka magharibi na kurudi nayo makwao wakati watu wetu wao walirudi na mashairi”  alisema mwalimu wetu mmoja.Nendeni magharibi mkachukue hazina  iliyopotea huko kwa miaka 200 ni hekaya nzuri inayosimuliwa kimtindo wa ushairi na Sezai Karakoç kumuhusu baba na watoto wake saba.  

Nenda magharibi ujifunze kwa ajili ya nchi yako

“Wanaotumwa katika mataifa haya ya magharibi wanatumwa kwa madhumuni kwamba  wachukue ujuzi unaopatikana huko kisha warudi katika nchi zao wachangie katika kuziendeleza nchi hizo”.Ingawa hayo ndio mategemeo lakini wanafunzi, wanataaluma, watafiti, wafanyakazi wa sekta ya umma na wengineo walio wengi inapofika muda wa kurudi makwao inakuwa ni suala gumu. Vyuo na na nchi zinazotuma watu wake ng’ambo vikifanya utafiti juu ya suala hilo vitagundua kuwa suala la kurudi makwao kwa wengi wa waliotumwa ni gumu.

Ni dhahiri wanafunzi, watafiti na wafanyakazi wa umma wanoelekea mataifa ya magharibi kwa madhumuni ya elimu haswa   elimu za jamii (social sciences) mara nyingi hujifunza vitu vinavyohusu nchi zile walizokwenda na sio nchi zao wanazotoka.

Ukiangalia ni hazina gani wataalamu hawa walioenda ng’ambo wakarudi, wamerudi nayo inatia huruma.

Iwe ni kwa manufaa ya nchi, sio kuwa mtaalamu mturuki kwa manufaa ya magharibi

Watu wengi wa jamii zisizokuwa za magharibi wanapoenda magharibi kwa ajili ya elimu, husukumwa na sababu mbalimbali. Wengine hutaka kujifunza masuala yanoyohusiana na nchi zao yaani malengo ni tofauti, baadhi ya watu matokeo huwa kinyume kabisa na matarajio.

Katika hali kama hii nchi hizi zinakuwa zimegawa fedha zake kuzipa nchi hizi za magharibi bila manufaa. Wasomi hawa wanachokisoma ng’ambo kinakuwa ni kwa manufaa ya mataifa hayo ya magharibi na sio kwenda kutatua matatizo ya nchi wanazotoka. Wanakuwa ni wataalamu waliobobea katika kutatua  mahitaji ya nchi za magharibi, ilhali wanahitajika watatue mahitaji ya nchi zao.

Tutolee mfano Uturuki, Kwa miaka 200 imekuwa ikituma watu nchi za magharibi kwa ajili ya elimu, Wengi wa watu wa taifa hili walitumwa mataifa kama Marekani, Ufaransa na Ujerumani. Lakkini hivi sasa wataalamu wetu kutoka mataifa hayo waliopo nchini Uturuki ni wachache sana.

Ni vigumu kukumkuta msomi kutoka magharibi akitumia vyanzo vya mashariki katika masuala ya magharibi lakini kwa Uturuki tumeona mara nyingi wataalamu  wakitumia vyanzo kama redio na televisheni za magharibi katika masuala mbalimbali yanayohusu Uturuki.

Inakuwa ni rahisi ukiangalia gharama na muda kwa nchi za magharibi kutumia watafiti wanaotoka mashariki, ambao wanamtazamo wa magharibi katika kufanya utafiti katika masuala ya kiorientali yanayohusu jamii, utamaduni, dini, makundi ya watu wachache na mada nyingine za kimkakati. Kwa hiyo hakuna haja tena ya kutuma watu kutoka magharibi kwenda kwenye jamii za mashariki kwa ajili ya tafiti hizi za kiorentalisti kwa kuwa wapo wanafunzi na watafiti kutoka mashariki wanaogharamikiwa na mataifa yao.

Maana mtafiti kutoka magharibi itabidi kwanza ajifunze lugha, ajifunze tofauti  zilizopo baina ya jamii hizi ,kitu ambacho kinachukua muda na gharama zaidi ukilinganisha na kuwatumia wataalamu kutoka mashariki wenye mtazamo wa kimagharibi wanaogharamikiwa na mataifa yao.

Kwa hiyo katika mada za kimkakati ambazo nchi za kimagharibi inaona kuna uhitaji huwatumia watu hawa jutoka mashariki ambao wamepandikizwa na kuaminishwa katika fikra na mitazamo ya  magharibi .

Na kiuhalisia hii ni akili kubwa sana imetumika kwa manufaa mapana ya jamii zao.

Je chanzo cha tatizo ni nchi wanazokwenda peke yake ?, Wiki ijayo tutaangalia tafiti zinazofanyika katika nchi za mashariki  kwa manufaa ya mataifa ya magharibi, elimu yenye lengo la kupotosha, na matokeo yenye lengo la kubadilisha mitizamo.

Ila kwa sasa tunaweza kusema kwamba chanzo cha tatizo sio nchi wanazoenda peke yake, yaani tatizo linachangiwa kwa kiasi kidogo sana na nchi za magharibi.

Maelezo ya mkuu wa kitivo cha elimu ya siasa wa chuo kikuu chaAnkara Yıldırım Beyazıt Prof. Dr. Kudret BÜLBÜLHabari Zinazohusiana